101
Zaburi ya Daudi. Nitaimba uaminifu wa agano lako na hukumu; kwako, Ee Yahwe, Nitakuimbia sifa. Nitatembea katika njia ya uadilifu. Oh, ni lini utakuja kwangu? Nitatembea kwa uadilifu ndani ya nyumba yangu. Sitaweka matendo maovu mbele ya macho yangu; ninachukia uovu usio na maana; hauta shikamana nami. Watu waliopotoka wataniacha mimi; mimi sichangamani na uovu. Nitamwangamiza yeyote amsengenyaye jirani yake kwa siri. Sitamvumilia yeyote mwenye kiburi. Nitawachagua walio waaminifu katika nchi wakae upande wangu. Wale watembeao katika njia ya uhadilifu watanitumikia. Watu wadanganyifu hawatabaki ndani ya nyumba yangu; waongo hawatakaribishwa mbele ya macho yangu. Asubuhi hata asubuhi nitawaangamiza waovu wote kutoka nchini; nitawaondoa watendao maovu wote katika mji wa Yahwe.