113
1 Msifuni Yahwe. Msifuni yeye, enyi watumishi wa Yahwe; lisifuni jina la Yahwe.
2 Litukuzwe jina la Yahwe, tangu sasa na hata milele.
3 Toka maawio ya jua hata machweo yake, Jina la Yahwe lazima lisifiwe.
4 Yahwe ameinuliwa juu ya mataifa yote, na utukufu wake wafika juu mbinguni.
5 Ni nani aliye kama Yahwe Mungu wetu, aliye na kiti chake juu,
6 atazamaye chini angani na duniani?
7 Humwinua maskini toka mavumbini na kumpandisha muhitaji kutoka jaani,
8 ili amketishe pamoja na wakuu, pamoja na wakuu wa watu wake.
9 Humpa watoto wanamke aliye tasa, humfanya yeye kuwa mama wa watoto mwenye furaha. Msifuni Yahwe!