112
1 Msifuni Yahwe. Amebarikiwa mtu yule anaye mtii Yahwe, apendezwaye sana na amri zake.
2 Kizazi chake kitakuwa ni chenye nguvu duniani; kizazi cha mcha Mungu kitabarikiwa.
3 Nyumbani mwake mna utajiri na mali; na haki yake itadumu milele.
4 Nuru huangazia gizani kwa ajili ya mtu mcha Mungu; yeye ni wa fadhili, huruma, na haki.
5 Heri atendaye fadhili na kukopesha, afanyaye mambo yake kwa uaminifu.
6 Kwa maana hataondoshwa kamwe; mwenye haki atakumbukwa milele.
7 Haogopi habari mbaya; ni jasiri, akimtumainia Yahwe.
8 Moyo wake ni mtulivu, hana woga, mpaka aonapo ushindi dhidi ya watesi wake.
9 Huwapa masikini kwa ukarimu; haki yake yadumu milele; atainuliwa kwa heshima.
10 Mtu mwovu ataona haya na kukasirika; atasaga meno yake na kuyeyuka; tamaa ya wasio haki itapotea.