116
1 Nampenda Yahwe kwa kuwa anasikia sauti yangu na kuomba kwangu kwa ajili ya huruma.
2 Kwa sababu alinisikiliza, nitamuita yeye ningali ninaishi.
3 Kamba za mauti zilinizunguka, na mitego ya kuzimu ilinikabili; niliona dhiki na huzuni.
4 Kisha niliita kwa jina la Yahwe: “Tafadhali Yahwe, uiokoe nafsi yangu.”
5 Yahwe ni mwenye neema na haki; Mungu wetu ni mwenye huruma.
6 Yahwe huwalinda wasio na hila; nilishushwa chini akaniokoa.
7 Nafsi yangu inaweza kurudi mahali pake pa kupumzika, kwa kuwa Yahwe amekuwa mwema kwangu.
8 Kwa maana uliokoa uhai wangu dhidi ya kifo, mcho yangu dhidi ya machozi, na miguu yangu dhidi ya kujikwaa.
9 Nitamtumikia Yahwe katika nchi ya walio hai.
10 Nilimwamini yeye, hata niliposema, “nimeteswa sana.”
11 Kwa haraka nilisema, “Watu wote ni waongo.”
12 Nimlipeje Yahwe kwa wema wake wote kwangu?
13 Nitakiinua kikombe cha wokovu, na kuliitia jina la Yahwe.
14 Nitatimiza viapo vyangu kwa Yahwe katika uwepo wa watu wake wote.
15 Mauti ya wacha Mungu ina thamani machoni pa Mungu.
16 Ee Yahwe, hakika, mimi ni mtumishi wako; mimi ni mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako; umefungua vifungo vyangu.
17 Nitakutolea dhabihu ya shukrani na nitaliitia jina la Yahwe.
18 Nitatimiza viapo vyangu kwa Yahwe katika uwepo wa watu wake wote,
19 katika nyua za nyumba ya Yahwe, katikati yako, Yerusalemu. Msifuni Yahwe.