138
Zaburi ya Daudi.
1 Nitakushukuru kwa moyo wangu wote; mbele ya miungu nitakuimbia sifa.
2 Nitasujundu mbele ya hekalu lako takatifu na kulishukuru jina lako kwa ajili ya uaminifu wa agano lako na kwa uaminifu wako. Umelifanya muhimu zaidi neno lako na jina lako kuliko kitu chochote.
3 Siku ile niliyo kuita, ulinijibu; ulinitia moyo na kuitia nguvu nafsi yangu.
4 Wafalme wote wa nchi watakushukuru wewe, Yahwe, maana watasikia maneno kutoka kinywani mwako.
5 Hakika, wataimba kuhusu matendo ya Yahwe, kwa kuwa utukufu wa Yahwe ni mkuu.
6 Maana ingawa Yahwe yuko juu, lakini anawajali wanyenyekevu, lakini hawatambui wenye majivuno.
7 Nijapopita katikati ya hatari, wewe utauhifadhi uhai wangu; utanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu, na mkono wako wa kuume utaniokoa.
8 Yahwe yuko pamoja nami hadi mwisho; uaminifu wa agano lako, Yahwe, wadumu milele. Usiwaache wale ambao mikono yako imewaumba.