5
Kwa kiongozi wa muziki; kwa vyombo vya upepo. Zaburi ya Daudi. Sikiliza nikuitapo, Yahweh; tazama kuugua kwangu. Sikiliza sauti yangu nikuitapo, Ee Mfalme wangu na Mungu wangu, kwa kuwa ni kwako Bwana naomba. Yahweh; sikia kilio changu asubuhi; na asubuhi nitaleta dua yangu kwako na kungoja kwa matarajio. Hakika wewe ni Mungu usiye kubaliana na uovu; watu waovu hawawezi kuwa wageni wako. Wenye kiburi hawata simama katika uwepo wako; wewe unawachukia wote wanaofanya maovu. Nawe utawaharibu waongo; Yahweh huwadharau vurugu na watu wadanganyifu. Lakini kwangu mimi, kwa sababu ya ukuu na uaminifu wa agano lako, nitakuja nyumbani mwako; na kwa heshima nitakuinamia mbele ya hekalu lako takatifu. Oh Bwana, uniongoze katika haki yako kwa sababu ya adui zangu; usawazishe njia yako mbele yangu. Kwa kuwa midomoni mwao hamna ukweli; utu wao wa ndani ni mwovu; makoo yao ni kaburi lililo wazi; husifu kinafiki kwa ulimi wao. 10 Mungu, wafanye kuwa na hatia; mipango yao iwe kuanguka kwao! Kwa ajili ya makosa yao mengi uwatoe nje, kwa kuwa wamekuasi wewe. 11 Bali wale wanao kukimbilia wafurahi; uwafanye wapige kelele kwa shangwe siku zote kwa sababu unawapigania; uwafanye wenye furaha ndani yako, wale walipendao jina lako. 12 Kwa maana utawabariki wenye haki, Yahweh; utawazunguka kwa neema kama ngao.