64
Kwa kiongozi wa muziki. Zaburi ya Daudi. Sikia sauti yangu, Mungu, usikilize malalamiko yangu; unilinde dhidi ya hofu ya adui zangu. Unifiche dhidi ya mipango ya siri ya wafanyao maovu, unifiche dhidi ya watendao vurugu ya udhalimu. Wao wamenoa ndimi zao kama panga; wamelenga mishale yao, maneno machungu, ili kwamba waweze kupiga kutoka mahali pa siri kwenda kwa mtu asiye na hatia; wampige yeye kwa ghafla nao wasihofu lolote. Wao wanahamasishana wenyewe katika kupanga uovu; wanashauriana pamoja wao binafsi ili kuweka mitego; nao husema, “Ni nani atakayetuona?” Wanabuni mipango ya dhambi; “Tumemaliza,” wanasema, “ni mpango makini.” Mawazo ya ndani na mioyo ya watu ni ya kina. Lakini Mungu atawapiga wao; ghafla watajeruhiwa kwa mishale yake. Watafanywa kuwa mashakani, kwa kuwa ndimi zao wenyewe ziko kinyume nao; wote wawaonao watatikisa vichwa vyao. Watu wote wataogopa na kutangaza matendo ya Mungu. Kwa hekima watafikiria kuhusu kile yeye ametenda. 10 Wenye haki watakuwa na furaha kuhusu Yahwe nao watakimbilia kwake; wote wenye haki moyoni watajivuna katika yeye.