95
Oh njoni, tumwimbie Yahwe; na tumwimbie kwa shangwe mwamba wa wokovu wetu. Tuingie uweponi mwake kwa shukrani; tumwimbie yeye kwa zaburi ya sifa. Kwa maana Yahwe ni Mungu mkuu na Mfalme mkuu juu ya miungu yote. Mkononi mwake zimo bonde za dunia; navyo vilele vya milima ni vyake. Bahari ni yake, maana aliiumba, na mikono yake ilitengeneza nchi kavu. Oh njoni, tumwabudu na tupige magoti; tupige magoti mbele za Yahwe, muumbaji wetu: Kwa maana yeye ni Mungu wetu, na sisi tu watu wa malisho yake na kondoo wa mkono wake. Ni heri leo mngesikia sauti yake! Msiifanye migumu mioyo yenu, kama vile huko Meriba, au kama ile siku ya Masa jangwani, ambako baba zenu walinijaribu na kunipima, japo walikuwa wameyaona matendo yangu. 10 Kwa miaka arobaini nilikasirishwa na kizazi hicho na kusema, 'Hawa ni watu ambao mioyo yao imepotoka; hawazijui njia zangu.' 11 Hivyo katika hasira yangu niliapa kwamba wasingeingia kamwe mahali pa pumziko.”