94
1 Yahwe, Ee Mungu ulipaye kisasi, Mungu ulipaye kisasi, utuangazie sisi.
2 Inuka, muhukumu wa nchi, uwape wenye majivuno kile wanachosahili.
3 Mpaka lini waovu, Yahwe, mpaka lini waovu watafurahia?
4 Wanamwaga maneno yao ya kiburi; wote watendao uovu wanajivuna.
5 Wanawaangamiza watu wako, Yahwe; wanalitesa taifa ambao ni milki yako.
6 Wanamuua mjane na mgeni aishiye nchini mwao, na wanamuua yatima.
7 Nao husema, “Yahwe hawezi kuona, Mungu wa Yakobo hayagundui haya.”
8 Tambueni, ninyi watu wajinga! Enyi wapumbavu, mtajifunza lini?
9 Yeye aliye liumba sikio, hasikii? Yeye aliye litengeneza jicho, haoni?
10 Yeye awaadhibuye mataifa, hayuko sahihi? Yeye ndiye ampaye maarifa mwanadamu.
11 Yahwe anayajua mawazo ya wanadamu, kuwa ni mvuke.
12 Amebarikiwa yule ambaye umuongozaye, Yahwe, yule ambaye wewe humfundisha kutoka katika sheria yako.
13 Wewe humpa pumziko wakati wa shida mpaka shimo litakapokuwa limechimbwa kwa ajili ya waovu.
14 Maana Yahwe hatawaacha watu wake wala kutelekeza warithi wake.
15 Kwa kuwa tena hukumu itakuwa ya haki; na wote walio wanyoofu wa moyo wataifuata.
16 Ni nani atainuka kunitetea dhidi ya watendao uovu? Ni nani atasimama dhidi ya waovu kwa ajili yangu?
17 Kama Yahwe asingelikuwa msaada wangu, haraka ningekuwa nimelala mahali pa ukimya.
18 Niliposema, mguu wangu unateleza,” Uaminifu wa agano lako, Yahwe, uliniinua.
19 Wasiwasi uwapo mwingi ndani yangu, faraja yako hunifurahisha.
20 Kiti cha uharibifu chaweza kushirikiana nawe, kitungacho madhara kwa njia ya sheria?
21 Wao kwa pamoja hupanga njama kuwaua wenye haki na kuwahukumu adhabu ya kifo wenye haki.
22 Lakini Yahwe amekuwa mnara wangu mrefu, na Mungu wangu amekuwa mwamba wa kimbilio langu.
23 Yeye atawarudishia uovu wao wenyewe na atawaangamiza katika uovu wao wenyewe. Yahwe Mungu wetu atawaangamiza.