98
Zaburi. Oh, mwimbieni Yahwe wimbo mpya, kwa kuwa ametenda mambo ya ajabu; mkono wake wa kuume na mkono wake mtakatifu vimempa ushindi. Yahwe ameufanya wokovu wake ujulikane; ameidhihirisha haki yake kwa mataifa yote. Hukumbuka uaminifu wa agano lake na uaminifu kwa ajili ya nyumba ya Israeli; miisho yote ya dunia itauona ushindi wa Mungu wetu. Mshangilieni Yahwe, nchi yote; pazeni sauti kwa wimbo, imbeni kwa furaha, na imbeni sifa. Mwimbieni Yahwe sifa kwa kinubi, kwa kinubi na wimbo wenye muiki wa kupendeza. Kwa panda na sauti ya baragumu, fanyeni kelele za shangwe mbele ya Mfalme, Yahwe. Bahari na ipige kelele na vyote vilivyomo, ulimwengu na wale wakaao ndani yake! Mito na ipige makofi, na milima ipige kelele kwa furaha. Yahwe anakuja kuihukumu nchi; naye ataihukumu dunia kwa haki na mataifa kwa adili.