99
Yahwe anatawala; mataifa na yatetemeke. Ameketi juu ya makerubi; nchi inatetemeka. Yahwe ni mkuu katika Sayuni; naye ametukuka juu ya mataifa yote. Nao walisifu jina lako kuu na lenye kutisha; yeye ni mtakatifu. Mfalme ana nguvu, naye hupenda haki. Wewe umeimarisha haki; umetenda haki na hukumu katika Yakobo. Msifuni Yahwe Mungu wetu na sujuduni miguuni pake. Yeye ni mtakatifu. Musa na Haruni walikuwa miongoni mwa makuhani wake, na Samweli alikuwa miongoni mwa wale walio muomba Yeye. Walimuomba Yahwe, naye akawajibu. Alizungumza nao toka nguzo ya wingu. Walizishika amri zake takatifu na sheria ambazo aliwapatia. Wewe uliwajibu, Yahwe Mungu wetu. Ulikuwa kwao Mungu mwenye kusamehe, lakini uliye adhibu matendo yao ya dhambi. Msifuni Yahwe Mungu wetu, na mwabuduni kwenye mlima wake mtakatifu, maana Yahwe Mungu wetu ni Mtakatifu.