30
1 Hzekia akatuma wajumbe kwa Israeli wote na Yuda, na pia akawaandikia barua Efraimu na Manase, kwamba waje kwenye nyumba ya Yahwe katika Yerusalemu, kusherekea Pasaka ya Yahwe, Mungu wa Israeli.
2 Kwa maana mfalme, viongozi wake, na kusanyiko lote katika Yerusalemu walikuwa wameshauriana pamoja, wakakubaliana kusherekea Pasaka katika mwezi wa pili.
3 Hawakuweza kuisherekea mapema kabla ya hapo, kwa sababu hapakuwa na makuhani wa kutosha waliojitakasa wenyewe, wala watu hawakuwa wamekusanyika pamoja Yerusalemu.
4 Pendekezo hili likaonekana sahihi katika macho ya mfalme na ya kusanyiko lote.
5 Kwa hiyo wakakubaliana kufanya tangazo katika Israeli yote, kuanzia Beer-sheba hadi Dani, kwamba watu lazima waje kusherehekea Paska ya Yahwe, Mungu wa Israeli, huko Yerusalemu. Kwa maana walikuwa hawakuwa wameisherehekea kwa hesabu kubwa ya watu, kwa mujibu wa jinsi ilivyokuwa imeandikwa.
6 Hivyo matarishi wakaenda na barua kutoka kwa mfalme na viongozi wake katika Israeli na Yuda yote, kwa agizo la mfalme. wakasema, “Ninyi watu wa Israeli, rudini kwa Yahwe, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Israeli, ili kwamba aweze kuwarudia masalia wenu ninyi mlipona kutoka kwenye mkono wa wafalme wa Ashuru.
7 Msiwe kama babu zenu au ndugu zenu, ambao walimuasi Yahwe, Mungu wa mababu zao, hivyo akawaweka katika kuangamia, kama mnavyoona.
8 Sasa msiwe wasumbufu, kama babu zenu walivyokuwa; badala yake, jitoeni wenyewe kwa Yahwe na njoeni kwenye sehemu yake takatifu, ambayo ameitakasa milele, na mwabuduni Yahwe Mungu wenu, ili kwamba uso wake wenye hasira uwageukie mbali.
9 Kwa maana ikiwa mtageuka nyuma kwa Yahwe, ndugu zenu na watoto wenu watapata huruma mbele ya hao wanaowaongoza kama wafungwa, na watarudi katika nchi hii. Kwa maana Yahwe Mungu wenu, ni mkarimu na mwenye huruma, na hatawageuzia mbali uso wake, kama mtarudi kwake.”
10 Kwa hiyo matarishi wakapita mji kwa mji katika majimbo ya Efraimu na Manase, njia yote hadi Zabuloni, lakini watu waliwacheka na kuwazomea.
11 Lakini, watu wengine wa Asheri na Manase na Zabuloni walijinyenyekesha wenyewe na wakaja Yerusalemu.
12 Mkono wa Mungu pia ukaja juu ya Yuda, kuwapa moyo mmmoja, ili kulikubali agizo la mfalme na viongozi kwa neno la Yahwe.
13 Watu wengi, kusanyiko kubwa, likakusanyika Yerusalemu kusherehekea Sikukuu ya Mikate Isiyochacha katika mwezi wa pili.
14 Waliinuka na kuchukua madhabahu zizilizokuwa Yerusalemu, madhabahu zote kwa ajili ya sadaka za kufukiza; wakazirusha katika kijito Kidroni.
15 Kisha wakamuua mwanakondoo wa Paska katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Makuhani na Walawi wakaona aibu, kwa hiyo wakajitakasa wenyewe na kuleta sadaka za kuteketezwa katika nyumba ya Yahwe.
16 Wakasimama katika sehemu zao katika makaundi yao, wakifuata maelekezo yaliyotolewa na sheria ya Musa, mtu wa Mungu. Makuhani wakainyunyiza damu waliyoipokea kutoka kwenye mikono ya Walawi.
17 Kwa maana walikuwepo wengi katika kusanyikao amaabao hawakuwa wamejitakasa wenyewe. Kwa hiyo Makuhani wakamchinja mwanakondoo wa Pasaka kwa ajili ya kila mmoja ambaye hakuwa amejisafisha na hakuweza kuzitakasa sadaka zake kwa Yahwe.
18 Kwa kuwa wingi wa watu, wengi wao kutoka Efraimu na Manase, Asakari na Zabuloni, hawakuwa wamejitakasa wenyewe, bado waliula mlo wa Paska, kinyume na maelekezo yaliyoandikwa. Kwa kuwa Hezekia alikuwa amewaombea, akisema, “Mungu Yahwe amsamehe kila mmoja
19 ambaye anaulekeza moyo wake kumtafuta Mungu, Yahwe, Mungu wa babu zake, hata kama hajasafiswa kwa utakaso wa viwango vya patakatifu.”
20 Kwa hiyo Yahwe akamsikiliza Hezekia na akawaponya watu.
21 Watu wa Israeli waliokuwepo Yerusalemu wakaitunza Sikukuu ya Mikaate Isiyochachwa na furaha kubwa kwa siku saba. Walawi na makuhani wakamsifu Yahwe siku baada ya siku, wakiimwimbia Yahwe kwa vyombo vya sauti kuu.
22 Hezekia akazungumza kwa kuwatia moyo Walawi wote walioilewa ibada ya Yahwe, Kwa hiyo wakala kwa kipindi cha siku saba, wakitoa sadaka za amani, na kufanya toba kwa Yahwe, Mungu wa babu zao.
23 Kusanyiko lote kisha likaamua kusherehekea kwa siku zingine saba, na wakafanya hivyo kwa furaha.
24 Kwa kuwa Hezekia mfalme wa Yuda aliwapa kusanyiko ng'ombe dume elf moja, na kondoo elfu saba kama sadaka; na viongozi wakawapa kusanyiko ng'ombe dume elfu moja na kondoo na mbuzi elfu kumi. Idadi kubwa ya makuhani wakajitakasa wenyewe.
25 Kusanyiko lote la Yuda, pamoja na makuhani na Walawi na watu wote walikuja pamoja kutoka nchi ya Israeli na wale walioishi Yuda—wote wakafurahia.
26 Hivyo kulikuwa na furaha kuu katika Yerusalemu, kwa kuwa tangu wakati wa Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli, hapakuwa na kitu kama hicho katika Yerusalemu.
27 Kisha makuhani, Walawi, wakainuka na kuwabariki watu. Sauti zao zilisikika na maombi yao yakaenda juu mbinguni, sehemu takatifu ambapo Mungu anaishi.