2
Kwa hiyo hauna udhuru, wewe uhukumuye, kwa maana katika yale uhukumuyo mwingine wajitia hatiani mwenyewe. Kwa maana wewe uhukumuye unafanya mambo yale yale. Lakini twajua kwamba hukumu ya Mungu ni ya kweli juu yao wafanyao mambo kama hayo. Lakini wewe tafakari hili, wewe ambaye unahukumu wale wanaotenda mambo hayo ingawa nawe unafanya mambo yayo hayo. Je utaepuka hukumu ya Mungu? Au unafikiri kidogo sana juu ya wingi wa wema wake, kuchelewa kwa adhabu yake, na uvumilivu wake? Je, hujui kwamba wema wake unapaswa kukuelekeza katika toba? Bali kwa kadiri ya ugumu wako na kwa moyo wako usio na toba wajiwekea mwenyewe akiba ya ghadhabu kwa siku ile ya ghadhabu, yaani, siku ile ya ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu. Yeye atamlipa kila mtu kipimo sawa na matendo yake: kwa wale ambao kwa uthabiti wa matendo mema wametafuta sifa, heshima na kutokuharibika, atawapa uzima wa milele. Lakini kwa wale ambao ni wabinafsi, wasioitii kweli bali hutii dhuluma, ghadhabu na hasira kali itakuja. Mungu ataleta dhiki na shida juu ya kila nafsi ya binadamu aliyefanya uovu, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia. 10 Lakini sifa, heshima na amani itakuja kwa kila mtu atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia. 11 Kwa maana hakuna upendeleo kwa Mungu. 12 Kwa maana kama vile wengi waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na kama vile wengi waliokosa kulingana na sheria watahukumiwa kwa sheria. 13 Maana si wasikiaji wa sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki. 14 Kwa maana watu wa Mataifa, ambao hawana sheria, wanafanya kwa asili mambo ya sheria, wao, wamekuwa sheria kwa nafsi zao, ingawa wao hawana sheria. 15 Kwa hili wanaonesha kwamba matendo yanayohitajika kwa mujibu wa sheria yameandikwa ndani ya mioyo yao. Dhamiri zao pia zinawashuhudia wao, na mawazo yao wenyewe ama huwashitaki au huwalinda wao wenyewe 16 na pia kwa Mungu. Haya yatatokea katika siku ambayo Mungu atazihukumu siri za watu wote, sawasawa na injili yangu, kwa njia ya Yesu Kristo. 17 Tuseme kwamba unajiita mwenyewe Myahudi, aliyekaa katika sheria, shangilia kwa kujisifu katika Mungu, 18 yajue mapenzi yake, na kupima mambo ambayo yanatofautiana nayo, baada ya kuagizwa na sheria. 19 Na tuseme kwamba una ujasiri kwamba wewe mwenyewe ni kiongozi wa kipofu, mwanga kwa wale walio gizani, 20 msahihishaji wa wajinga, mwalimu wa watoto, na kwamba unayo katika sheria jinsi ya elimu na kweli. 21 Wewe basi, uhubiriye mwingine, je, hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kutokuiba, je wewe huiba? 22 Wewe usemae usizini, je unazini? Wewe uchukiaye sanamu, je unaiba hekaluni? 23 Wewe ujisifuye katika sheria, je haumfedheheshi Mungu katika kuvunja sheria? 24 Kwa maana “jina la Mungu linafedheheshwa kati ya watu wa mataifa kwa sababu yenu,” kama ilivyoandikwa. 25 Kwa maana Kutahiriwa kweli kwafaa kama ukitii sheria, lakini kama wewe ni mkiukaji wa sheria, kutahiriwa kwako kunakuwa kutokutahiriwa. 26 Basi, ikiwa, mtu asiyetahiriwa anaendelea kushika matakwa ya sheria, je kutokutahiriwa kwake hakutachukuliwa kana kwamba ametahiriwa? 27 Na yeye asiyetahiriwa kwa asili hatakuhukumu kama akitimiza sheria? Hii ni kwa sababu una maandiko yaliyoandikwa na tohara pia lakini bado u mkiukaji wa sheria! 28 Kwa maana yeye si Myahudi aliye kwa hali ya nje; wala kutahiriwa si kule ambako ni kwa nje tu katika mwili. 29 Lakini yeye ni Myahudi aliye kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko. Sifa ya mtu wa namna hiyo haitokani na watu bali yatoka kwa Mungu.