1Timotheo
1
1 Paulo, Mtume wa Kristo Yesu, kulingana na amri ya Mungu na Mwokozi wetu Yesu Kristo aliye ujasiri wetu,
2 kwa Timotheo mwanangu wa kweli katika imani: Neema, rehema na amani zitokazo kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu.
3 Kama nilivyokusihi nilipoondoka kwenda Makedonia, ubaki Efeso ili kwamba uweze kuwaamru watu fulani wasifundishe mafundisho tofauti.
4 Pia wasisikilize hadithi na orodha za nasaba zisizo na mwisho. Haya husababisha mabishano zaidi kuliko kuwasaidia kuendeleza mpango wa Mungu wa imani.
5 Basi lengo la agizo hili ni upendo utokao katika moyo safi, katika dhamiri nzuri na katika imani ya kweli.
6 Baadhi ya watu wamelikosa lengo wakayaacha mafundisho haya na kugeukia mazungumzo ya kipumbavu.
7 Wanataka kuwa waalimu wa sheria, lakini hawafahamu wanachosema au wanachosisitiza.
8 lakini tunajua kwamba sheria ni njema kama mtu ataitumia kwa usahihi.
9 Tunajua kuwa, sheria haikutungwa kwa ajili ya mtu mwenye haki, bali kwa ajili ya wavunja sheria na waasi, watu wasio wataua na wenye dhambi, na ambao hawana Mungu na waovu. Imetungwa kwa ajili ya wauao baba na mama zao, kwa ajili ya wauaji,
10 kwa ajili ya waasherati, kwa ajili ya watu wazinzi, kwa ajili ya wale wanaoteka watu na kuwafanya watumwa, kwa ajili ya waongo, kwa ajili ya mashahidi wa uongo, na yeyote aliye kinyume na maelekezo ya uaminifu.
11 Malekezo haya yanatokana na injili yenye utukufu ya Mungu mwenye kubarakiwa ambayo kwayo nimeaminiwa.
12 Ninamshukuru Yesu Kristo Bwana wetu. Alinitia nguvu, kwa kuwa alinihesabu mimi kuwa mwaminifu, na akaniweka katika huduma.
13 Nilikuwa mtu wa kukufuru, mtesaji na mtu wa vurugu. Lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda kwa ujinga kwa kutoamini.
14 Lakini neema ya Mungu wetu imejaa imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.
15 Ujumbe huu ni wa kuaminika na unastahili kupokelewa na wote, ya kuwa Kristo Yesu alikuja duniani kuokoa wenye dhambi. Mimi ni mbaya zaidi ya wote.
16 Lakini kwa sababu hii mimi nilipewa rehema ili kwamba ndani yangu mimi, awali ya yote, Kristo Yesu adhihirishe uvumilivu wote. Alifanya hivyo kama kielelezo kwa wote watakaomtumaini Yeye kwa ajili ya uzima wa milele.
17 Na sasa kwa Mfalme asiye na ukomo, asiyekufa, asiyeonekana, Mungu pekee, iwe heshima na utukufu milele na milele. Amina.
18 Ninaliweka agizo hili mbele yako Timotheo, mtoto wangu. Nafanya hivi kulingana na unabii uliotolewa hapo kwanza kukuhusu wewe, ili kwamba uhusike katika vita njema.
19 Fanya hivyo ili kwamba uwe na imani na dhamiri njema. Baadhi ya watu wameyakataa haya wakaangamiza imani.
20 Kama vile Himeneyo na Alekizanda ambao nimempa shetani ili wafundishwe wasikufuru.