2
1 Kwa hiyo awali ya yote, nahitaji maombi, na dua, na maombezi, na shukrani vifanyike kwa ajili ya watu wote,
2 kwa ajili ya wafalme na wote ambao wako kwenye mamlaka, ili kwamba tuweze kuishi maisha ya amani na utulivu katika utauwa wote na heshima.
3 Hili ni jema na lenye kukubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu.
4 Yeye hutamani kuwa watu wote waokolewe na wapate kuijua kweli.
5 Kwa kuwa kuna Mungu mmoja, na kuna mpatanishi mmoja kati ya Mungu na mwanadamu ambaye ni Kristo Yesu.
6 Alijitoa mwenyewe kama fidia kwa wote, kama ushuhuda kwa wakati muafaka.
7 Kwa sababu hii, mimi mwenyewe nilifanywa kuwa mjumbe wa injili na mtume. Nasema kweli. Sisemi uongo. Mimi ni mwalimu watu Mataifa katika imani na kweli.
8 Kwa hiyo, nataka wanaume kila mahali waombe na kuinua mikono mitakatifu bila ghadhabu na mashaka.
9 Vivyo hivyo, nataka wanawake wajivike mavazi yanayokubalika, kwa heshima na kujizuia. Wasiwe na nywele zilizosukwa, au dhahabu, au Lulu, au mavazi ya gharama kubwa.
10 Pia nataka wavae mavazi yanayowastahili wanawake wanaokiri uchaji kwa kupitia matendo mema.
11 Mwanamke na ajifunze katika hali ya utulivu na kwa utii wote.
12 Simruhusu mwanamke kufundisha, au kuwa na mamlaka juu ya mwanaume bali aishi katika hali ya ukimya.
13 Kwa kuwa Adamu aliumbwa kwanza, kisha Eva.
14 Adamu hakudanganywa, lakini mwanamke alidanganywa kabisa katika uasi.
15 Hata hivyo, ataokolewa kwa kupitia kuzaa watoto, kama wataendelea katika imani na upendo na katika utakaso na akili njema.