*
Zaburi 112
Baraka Za Mwenye Haki
Msifuni Bwana.
 
Heri mtu yule amchaye Bwana,
mtu yule apendezwaye sana na amri zake.
 
Watoto wake watakuwa wenye uwezo katika nchi,
kizazi cha watu waadilifu kitabarikiwa.
Nyumbani mwake kuna mali na utajiri,
haki yake hudumu milele.
Hata gizani nuru humzukia mtu mwadilifu,
yule mwenye rehema, huruma na haki.
 
Mema yatamjia mtu yule aliye mkarimu na mwenye kukopesha bila riba,
anayefanya mambo yake kwa haki.
Hakika hatatikisika kamwe,
mtu mwenye haki atakumbukwa milele.
Hataogopa habari mbaya,
moyo wake ni thabiti, ukimtegemea Bwana.
Moyo wake ni salama, hatakuwa na hofu,
mwishoni ataona ushindi dhidi ya adui zake.
Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu akawapa maskini;
haki yake hudumu milele;
pembe yake itatukuzwa kwa heshima.
 
10 Mtu mwovu ataona na kuchukizwa,
atasaga meno yake na kutoweka,
kutamani kwa mtu mwovu kutaishia patupu.
* Zaburi 112: Zaburi hii imetungwa kila mstari ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.