Zaburi 126
Kurejezwa Kutoka Utumwani
Wimbo wa kwenda juu.
Bwana alipowarejeza mateka Sayuni,
tulikuwa kama watu walioota ndoto.
Vinywa vyetu vilijaa kicheko,
ndimi zetu zilijaa nyimbo za shangwe.
Ndipo iliposemwa miongoni mwa mataifa,
Bwana amewatendea mambo makuu.”
Bwana ametutendea mambo makuu,
nasi tumejaa furaha.
 
Ee Bwana, turejeshee watu wetu waliotekwa,
kama vijito katika Negebu.
Wapandao kwa machozi
watavuna kwa nyimbo za shangwe.
Yeye azichukuaye mbegu zake
kwenda kupanda, huku akilia,
atarudi kwa nyimbo za shangwe,
akichukua miganda ya mavuno yake.