121
Wimbo wa kwenda hekaluni kuabudu. Nitayainua macho yangu nitazame milimani. Msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu unatoka kwa Yahwe, aliyezifanya mbingu na nchi. Hatauacha mguu wako uteleze; yeye akulindaye hatasinzia. Tazama, mlinzi wa Israeli hatasinzia wala hatalala usingizi kamwe. Yahwe ni mlinzi wako; Yahwe ni uvuli mkono wako wa kuume. Jua halitakudhuru wakati wa mchana, wala mwezi wakati wa usiku. Yahwe atakulinda na madhara yote, na ataulinda uhai wako. Yahwe atakulinda katika yote ufanyayo sasa na hata milele.