69
Kwa kiongozi wa muziki; seti kwenye Shoshannim. Zaburi ya Daudi.
1 Uniokoe, Mungu; maana maji yameweka uhai wangu hatarini.
2 Ninazama kwenye kina cha matope, pasipo na hahari pa kusimama; nimekuja kwenye kina kirefu cha maji, ambako mafuriko yananifunika.
3 Nimechoka sana kwa kulia kwangu; koo langu ni kavu; macho yangu yanafifia wakati namngoja Mungu wangu.
4 Wale wanichukiao bila sababu wako zaidi ya nywele za kichwa changu; wale ambao wangeweza kuniua, wakiwa adui zangu kwa sababu zisizo sahihi, ni wengi mno; wanalazimisha nirudishe kile ambacho sijaiba.
5 Mungu, wewe unaujua ujinga wangu, na dhambi zangu hazifichiki kwako.
6 Usiwaache wale wanao kungoja wewe waaibishwe kwa sababu yangu, Bwana Yahwe wa majeshi; usiwaache wale wanaokutafuta wewe wadharauliwe kwa sababu yangu, Mungu wa Israeli.
7 Kwa ajili yako nimestahimili lawama; aibu imeufunika uso wangu.
8 Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, nisiye fahamika wala kuaminika kwa watoto wa mama yangu.
9 Kwa maana bidii ya nyumba yako imenila, na laumu zao wanao kulaumu wewe zimeniangukia mimi.
10 Wakati nilipolia na kutokula chakula, walinitukana.
11 Nilipoteneneza mavazi ya gunia, nikawa kituko kwao.
12 Wale wakaao katika lango la mji huniseng'enya; mimi ni wimbo wa walevi.
13 Lakini kwangu mimi, maombi yangu ni kwako, Yahwe, wakati ambao wewe utayapokea; unijibu katika uaminifu wa wokovu wako.
14 Unitoe matopeni, na usiniache nizame; uniondoe mbali na wale wanaonichukia na uniokoe katika kina cha maji.
15 Usiache mafuliko ya maji yanielemee, wala kina kisinimeze. Usiache mdomo wa shimo unimeze.
16 Unijibu, Yahwe, maana uaminifu wa agano lako ni mwema; kwa maana rehema zako kwangu ni nyingi, unigeukie.
17 Usiufiche uso wako mbali na mtumishi wako, maana niko katika dhiki; unijibu haraka.
18 Uje kwangu na unikomboe. Kwa sababu ya adui zangu, uwe fidia yangu.
19 Wewe wajua kulaumiwa kwangu, kuaibishwa kwangu, na kudharauliwa kwangu; wapinzani wangu wote wako mbele yako.
20 Lawama imevunja moyo wangu; nimejawa na huzuni kubwa; nilitafuta mtu wa kunihurumia, lakini hakuwepo; nilitafuta wafariji, lakini sikupata.
21 Walinipa sumu kwa ajili ya chakula changu; katika kiu yangu walinipa siki ninywe.
22 Meza yao mbele yao na iwe mtego; wafikiripo wako kwenye usalama, iwe kitanzi.
23 Macho yao na yatiwe giza ili kwamba wasiweze kuona; uvifanye viuno vyao kutetemeka daima.
24 Wamwagie gadhabu yako, ukali wa hasira yako uwafikie wao.
25 Sehemu yao na iwe ukiwa; mtu yeyote asiishi katika hema yao.
26 Kwa kuwa walimtesa yule uliyempa adhabu. Mara kwa mara walihesabu maumivu ya wale walioumizwa.
27 Wakiwashtaki kuwa wamefanya uovu juu ya uovu; usiwaache waje kwenye ushindi wa haki yako.
28 Uwafute kwenye Kitabu cha Uzima na wasiandikwe pamoja na wenyehaki.
29 Lakini mimi ni maskini na mwenye huzuni; uruhusu wokovu wako, Mungu, uniweke juu sana.
30 Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo na nitamtukuza yeye kwa shukrani.
31 Nitamsifu Yahwe zaidi kuliko ng'ombe au ndama aliye na mapembe na kwato.
32 Wanyenyekevu wameona na kufurahi; ninyi mnao matafuta Mungu, mioyo yenu itiwe nguvu.
33 Maana Yahwe husikia wenye uhitaji naye hawadharau wafungwa wake.
34 Mbingu na nchi zimsifu yeye, bahari na vyote vitembeavyo majini.
35 Kwa maana Mungu ataiokoa Sayuni na ataujenga tena mji wa Yuda; watu wataishi huko na kupata umiliki wao.
36 Ukoo wa watumishi wake watairithi; nao walipendao jina lake wataishi humo.