90
Maombi ya Musa mtu wa Mungu.
1 Bwana, wewe umekuwa kimbilio letu vizazi vyote.
2 Kabla milima haijaumbwa, wala haujaumba nchi na dunia, tangu milele na milele, wewe ni Mungu.
3 Humrudisha mtu mavumbini, na kusema, “Rudi, ewe uzao wa mwanadmu.
4 Kwa maana miaka elfu machoni pako ni kama jana ipitapo, na kama saa wakati wa usiku.
5 Huwafagia kama vile kwa mafuliko nao hulala; na wakati wa asubuhi wako kama majani yameayo.
6 Asubuhi yachipuka na kumea; jioni yakatika na kukauka.
7 Hakika, tumeangamizwa kwa hasira yako, na gadhabu yako inatuogopesha sana.
8 Umeudhihirisha uovu wetu mbele zako, na dhambi zetu zilizofichika katika nuru ya uwepo wako.
9 Uhai wetu unatoweka chini ya gadhabu yako; Miaka yetu inapita haraka kama pumzi.
10 Miaka yetu ni sabini, au themanini tukiwa na afya; lakini hata hivyo miaka yetu mizuri imetiwa alama ya taabu na huzuni. Ndiyo, inapita haraka, kisha tunatoweka.
11 Ni nani ajuaye kiwango cha hasira yako, na ghadhabu yako ambayo iko sawa na hofu yako?
12 Hivyo utufundishe sisi kuyafikiria maisha yetu ili kwamba tuweze kuishi kwa hekima.
13 Ugeuke, Ee Yahwe! Mpaka lini itakuwa hivi? Uwahurumie watumishi wako.
14 Ututosheleze sisi wakati wa asubuhi kwa uaminifu wa agano lako ili kwamba tuweze kufurahi na kushangilia siku zote za maisha yetu.
15 Utufurahishe kwa uwiano sawa na zile siku ulizo tutesa na kwa ile miaka tuliyopitia taabu.
16 Watumishi wako na waione kazi yako, na watoto wetu wauone ukuu enzi yako.
17 Na neema ya Bwana Mungu wetu iwe yetu; fanikisha kazi za mikono yetu; hakika, fanikisha kazi ya mikono yetu.